Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shaaban amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Jumuiya ya Madola katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa rasilimali za ndani kupitia mifumo ya kisasa ya ukusanyaji kodi na ukaguzi wa forodha (IDRAS na TANCIS), pamoja na utekelezaji wa Mkakati wa Kipindi cha Kati wa Mapato.
Bi. Amina amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika kikao cha Jukwaa la Kimataifa linalowakutanisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Finance Ministers Meeting, CFMM 2025), kilichofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Aidha alibainisha kuwa dhamira ya Tanzania ya kuendeleza uchumi wenye utofauti ukiwa na uwekezaji katika utalii, teknolojia ya habari na mawasiliano, ubunifu wa kijani, na madini endelevu.
Ushirikiano wa kibiashara na Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati pamoja na sera za kibiashara za kikanda na mikakati ya uwekezaji kutoka diaspora unachukuliwa kuwa muhimu.
Bi Amina alimalizia kwa kuthibitisha dhamira ya Tanzania kushirikiana na wanachama wa Jumuiya ya Madola katika kufanikisha malengo ya uhimilivu wa kiuchumi, ukuaji jumuishi, na maendeleo endelevu, huku akisisitiza thamani ya msaada wa kiufundi na mazungumzo ya sera yanayopatikana kupitia jukwaa hili.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto za uchumi wa dunia na kutafuta mikakati ya kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi katika nchi wanachama.