Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-maamry Mwamba amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kufanya mageuzi ya kiuchumi na kijamii kwa faida ya wananchi na taifa kwa ujumla kupitia program mbalimbali zinazofadhiliwa na Shirika hilo.
Dkt. Natu Mwamba ametoa shukran hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika hilo Bw. Adran Ubisse Makao Makuu ya Taasisi hiyo Jijini Washington D.C nchini Marekani.
Aidha Dkt. Mwamba alimhakikishia kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika katika robo ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2025-2026 kwa kufikia asilimia 5.8 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho katika Mwaka wa Fedha uliopita 2024 pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei ambao umebaki katika wigo wa tarakimu moja wa asilimia tatu huku ikiwa na fedha za kutosha za kigeni hatua iliyosababishwa na usimamizi mzuri wa sera za uchumi na fedha pamoja na kuimarika kwa sekta za madini, nishati na shughuli za huduma na bidhaaza kifedha.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Adran Ubisse alisema kuwa Tanzania inarekodi nzuri ya utekelezaji wa miradi kwa kutumia vizuri fedha inazokopa.
Alisema kuwa Misaada ya kifedha na ya kiufundi inayopata Tanzania katika maendeleo mbalimbali sera nzuri usimamizi wa deni na masuala ya fedha inaifanya Tanzania kuwa ni moja ya nchi ambayo IMF imekuwa ukiitolea mfano kwa nchi nyingine ambapo mfano mzuri ni utekelezaji wa Mkakati wenu wa Maendeleo wa muda wa Kati unaosaidiwa kuutekeleza kupitia ufadhili wa IMF na nchi nyingine wadau wa maendeleo ambao unaiwezesha Tanzania kuimarisha ukusanyaji wa mapato yake ya ndani.
Hata hivyo mkutano huo wa uwili (bilateral meeting) imewashirikisha pia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu-Ofisi ya Rais Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mhe. Dkt. Elsie Kanza pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.