Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imetangaza kuwakamata watu wanane wa shirika la misaada ya kibinadamu, wakiwemo raia watatu wa Ulaya, kwa tuhuma za ujasusi na uhaini.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana, amesema waliokamatwa ni wanachama wa shirika la INSO lenye makao yake nchini Uholanzi, linalojihusisha na usalama wa mashirika ya misaada. Miongoni mwao ni raia wa Ufaransa, mwanamke mwenye uraia wa Ufaransa na Senegal, raia wa Jamhuri ya Czech, raia wa Mali, na Waburkina Faso wanne. Wengine ni mkurugenzi wa shirika hilo nchini Burkina Faso na naibu wake. Mkurugenzi huyo alishawahi kukamatwa mwishoni mwa Julai, wakati shirika hilo liliposimamishwa kwa miezi mitatu kwa madai ya kukusanya taarifa nyeti bila kibali. Tangu mapinduzi ya Septemba 2022, utawala wa kijeshi wa Burkina Faso imeachana na ushirikiano wa karibu na nchi za Magharibi, hasa Ufaransa.