Rais Macron akabiliwa na shinikizo la kujiuzulu

Aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, katika hatua ya kushangaza, amemtaka kiongozi huyo ajiuzulu kuinusuru nchi hiyo kutumbukia zaidi katika mzozo wa kisiasa

Wito wa Eduard Philipe, waziri mkuu aliyedumu kwa muda mrefu kwenye serikali ya Macron kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 na ambapo sasa ni kiongozi wa moja ya chama mshirika na kile cha Macron, umeongeza shinikizo kwa kambi ya rais Macron.

Kauli yake ameitoa siku moja kupita tangu Sebastien Lecornu, waziri mkuu mwingine aliyeteuliwa na Macron, kujizulu hapo jana ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu alipochukua wadhifa huo, uamuzi wake pia ukizidisha sintofahamu ya kisiasa kwenye taifa hilo.

Aidha Jumatatu ya wiki hii rais Macron, alimuagiza Lecornu, kuandaa mpango mkakati ambao utasaidia kutuliza joto la kisiasa, wakati huu wapinzani wake wakiongeza shinikizo la kumtaka ajiuzulu.

Uchaguzi ujao wa urais nchini Ufaransa umepangwa kufanyika mwaka 2027, lakini mvutano wa kisiasa unaoendelea kulikumba taifa hilo, huenda ukalazimisha kufanyika kwa uchaguzi mwingine baada ya ule uliofanyika mwaka 2024 baada ya kutokea sintofahamu nyingine ya kisiasa.

Wadadisi wa mambo wanasema ikiwa rais Macron ataamua kujiuzulu kitu ambacho hawaoni akikifanya, basi hataruhusiwa kugombea kwa muhula watatu hadi mwaka 2032.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii