Rais wa Madagascar Andry Rajoelina, amemteua Jenerali wa jeshi Ruphin Fortunat Dimbisoa Zafisambo, kuwa Waziri Mkuu mpya, wakati huu kisiwa hicho kinachoendelea kukabiliwa na maandamano ya vijana.
Uteuzi wa Jenerali Zafisambo, unalenga kutuliza maandamano ambayo yamekuwa yakiendelea dhidi ya serikali, ambapo vijana wa Gen Z, wanalalamilia uhaba wa maji na kukatika kwa umeme wa mara kwa mara nchini humo.
Mbali na madai hayo, waandamanaji sasa wanamtaka rais Rajoelina kujiuzulu urais, shinikizo ambazo pia zinaungwa mkono na wanasiasa wa upinzani.
Waandamanaji hao, wanaendelea kusisitiza kuwa, wataendelea na maandamano hadi pale rais Rajoelina atakapoondoka madarakani, huku wakimpa saa 48 kwa Waziri Mkuu mpya, kushughulikia madai yao.
Wiki iliyopita, rais Rajoelina aliwafuta kazi Mawaziri wake wote, lakini hatua hiyo haijawaridhisha waandamanaji ambao wameapa kuendelea kuandamana.