WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote hapa duniani kwani ndio wanaotoa rasilimaliwatu yenye elimu ambayo ni muhimu zaidi ya Taifa.
Amesema kuwa mafanikio ya kielimu, kijamii na kiuchumi yanatokana na juhudi za walimu kwani walimu ni fahari ya familia, jamii na nchi na kupitia mikono yao vijana wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi na maadili ya uzalendo.
Amesema hayo leo Ijumaa Oktoba 03 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya siku mwalimu duniani ambayo kiwilaya imeadhimishwa Bukombe mkoani Geita katika uwanja wa shule ya sekondari ya ushirombo.
"Kila hatua ya ustawi wa kijamii na kiuchumi inaanzia darasani kupitia juhudi na maarifa ya walimu. bila walimu, hakuna taaluma, hakuna viongozi wa kesho na hakuna Taifa linaloweza kusimama imara, walimu ndio chimbuko la uvumbuzi na ubunifu wa kizazi kipya.".
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada ya ualimu hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kada hiyo ikiwemo kwa kupandisha madaraja na kuimarisha mafunzo kwa walimu.
Ameongeza kuwa ili kukabiliana na upungufu wa walimu nchini Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuthamini na kuwekeza katika kada ya ualimu kwa kuajiri walimu wapya kila mwaka.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi ya Rais - UTUMISHI kufanya msawazo wa walimu ndani ya mikoa husika kwa kuhakikisha kila shule inapata walimu ili watoto wa kitanzania wapate elimu bora.
"Taaluma ya ualimu humfanya mtu kuwa raia mwema kwenye nchi na zaidi sana humfanya kuwa mtumishi, mfanyakazi na mzalishaji mali bora, wakati wote wa maisha yake, hii ni taaluma ambayo tunaamini ni ya uumbaji wa pili baada ya mwanadamu kuzaliwa na wazazi wake, kazi ya pili huendelea hapa duniani na muumbaji huwa ni mwalimu".