Vijana waliokuwa wamefunika nyuso zao wamekabiliana na polisi na kusababisha uharibifu wa mali katika miji kadhaa nchini Morocco wakati maandamano ya kuipinga serikali yakiendelea kwa siku ya tano mfululizo.
Maandamano hayo yaliyoanza Jumamosi iliyopita, yamekuwa yakilenga kudai maboresho katika sekta ya elimu na huduma za afya.
Aidha yameandaliwa kupitia mitandao ya kijamii na kundi la vijana linalojiita GenZ 212, ambalo limekuwa likitumia majukwaa kama TikTok, Instagram, na programu ya michezo mtandaoni ya Discord kuhamasisha uungwaji mkono.
Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Takwimu nchini Morocco, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa ujumla ni asilimia 12.8, huku ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana ukifikia asilimia 35.8, na asilimia 19 miongoni mwa wahitimu wa vyuo vikuu.a
Harakati za GenZ 212 zimechochewa na maandamano ya vijana yaliyofanyika hivi karibuni katika mataifa ya Asia na Amerika ya Kusini, yakionyesha msukumo wa kimataifa wa kizazi kipya kushinikiza mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kupitia nguvu ya mitandao ya kijamii.