Maandamano makubwa yamezuka nchini Italia kufuatia hatua ya Israel kuzuia msafara wa meli uliokuwa umebeba misaada kuelekea ukanda wa Gaza.
Mjini Rome, maelfu ya waandamanaji walikusanyika jana jioni nje ya kituo kikuu cha reli mjini humo. Mamlaka zililazimika kufunga kwa muda mlango wa kituo hicho pamoja na kufunga kituo cha karibu cha treni ya chini kwa chini kama tahadhari.
Kwa mujibu wa gazeti la La Repubblica, kundi la waandamanaji lilielekea katika ofisi ya Waziri Mkuu Giorgia Meloni na kuishtumu serikali yake ya mrengo wa kulia kwa kushindwa kuonyesha mshikamano na wanaharakati waliokuwemo ndani ya msafara huo wa meli
Shirika la Habari la ANSA limeripoti kuwa katika mji wa kusini wa Napoli, waandamanaji waliziba njia za reli katika kituo kikuu cha treni na kulazimisha huduma za usafiri wa treni kusitishwa kwa muda.
Maandamano mengine pia yameripotiwa katika miji ya kaskazini ya Milan na Turin, na kuonyesha kuenea kwa hasira ya umma dhidi ya Israel.
Wakati huo huo, chama kikubwa zaidi cha wafanyikazi nchini Italia, CGIL, kimetangaza mgomo wa kitaifa mnamo siku ya Ijumaa, kama ishara ya kuunga mkono maandamano hayo na kulaani kile kinachoonekana kama ukosefu wa mshikamano na wanaharakati waliokuwemo ndani ya msafara huo wa meli.