TRA kudhibiti ubora wa bidhaa kidigitali

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepata mwarobaini wa kukabiliana na changamoto ya utambuzi wa bidhaa bandia baada ya kutangaza rasmi programu tumizi ya ‘Hakiki Stempu’.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Februari 14, 2022 na mamlaka hiyo, mwananchi yeyote atalazimika kupakua programu hiyo katika simu yake ya kiganjani inayohusisha takribani nusu ya watanzania wanatumia intaneti kama inavyoelezwa katika ripoti za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata kupitia taarifa hiyo ametoa wito huo akisema lengo la kuanzisha mfumo huo ni kulinda afya za watumiaji dhidi ya bidhaa bandia ikiwa ni matokeo ya uwekezaji uliofanyika katika maboresho ya mifumo yake ya Tehama.

“Itawawezesha (App) kutambua bidhaa isiyofaa kwa matumizi na usalama wa afya zao pamoja na kuiwezesha serikali kukusanya kodi stahiki na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii kwa manufaa ya wananchi,” inanukuu taarifa ya kamishna huyo.

Kidata amesema maboresho mengine katika mifumo yamefanyika katika Stempu za Kielektroniki (ETS), alama maalumu inayobandikwa au kuchapishwa katika bidhaa ili kuhalalisha bidhaa iliyozalishwa au kuingizwa nchini na mfanyabiashara anayetambulika, akiwa amelipa kodi ya ushuru wa bidhaa stahiki.

“Vile vile TRA inatoa wito kwa wazalishaji na waingizaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa kwa kutumia mfumo wa ETS kuwa waaminifu kwani mfumo huo una faida nyingi kwao ikiwamo kulinda bidhaa zao sokoni dhidi ya bidhaa bandia pamoja na kusaidia makadirio ya kodi kwa haki.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii