Ajiua Chumbani kwa Mpenzi Wake Baada ya Kufukua Kaburi la Mama Yake

Mkazi wa Mpanda Hotel Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi Wille Mwakapimba amekutwa akiwa amejinyonga chumbani kwa mpenzi wake Hawa Ayubu na kuacha ujumbe ulioandikwa kuwa alisikia ujumbe wa sauti ya Mama yake (Mzimu) ambaye ni marehemu ikimtaka aende kufukua kaburini kwake( kaburi la mama yake) lililopo makaburi ya Mwangaza kwamba kuna vitu vya kishirikina vimefukiwa kwenye kaburi hilo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivukoni Kata ya Shanwe Michael Sikenyenzi amesema kuwa tukio la mtu huyo kujinyonga limetokea jana Jumapili Februari 13,2022 majira ya saa nne na robo asubuhi huko Kata ya Shanwe Manispaa ya Mpanda muda mfupi baada ya marehemu kutoka kituo cha Polisi Wilaya ya Mpanda.

Alisema kuwa taarifa za tukio hilo alizipata baada ya kupigiwa simu iliyomtaka kwende nyumbani kwa Hawa Ayubu kuna tukio la mtu kujinyonga nyumbani kwa mwanamke huyo .

Amebainisha kuwa baada ya kufika nyumbani kwa Hawa alikuta mwili wa marehemu huyo akiwa amejinyonga chumbani hali iliyomlazimu kutoa taarifa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi ambao walifika haraka eneo la tukio.

Sikenyenzi aliongeza kuwa baada ya Polisi kufika eneo la tukio waliingia chumbani na kukuta ujumbe wa maandishi aliokuwa ameandika marehemu ambao ulikuwa ukieleza kuwa alisikia sauti ya marehemu mama yake aende kwenye kaburi lake (marehemu mama yake) akafukue kuna vitu vimefukiwa na ndugu yake ambaye amekuwa akiwafanyia ushirikina ndugu zake.

Alisema baada ya kusoma barua hiyo waliwahoji ndugu wa marehemu waliokuwa wamefika kwenye eneo hilo akiwepo kaka yake mkubwa wa marehemu ambaye alidai kuwa ni kweli marehemu huyo alikwenda kwenye makaburi ya Mwangaza na kufukua na kukuta kichwa kinachosadikiwa cha binadamu na sehemu ya siri ya mwanamke sanda na kitambaa chekundu ambavyo alivichukua na kuvipeleka dukani kwa ndugu yake aliyekuwa akimtuhumu kuwa ni mshirikina ambapo alilitupa na kumwambia chukua mzigo wako ua wengine mimi huniwezi.

Alieleza kuwa baada ya kuwa amevipeleka vitu hivyo hapo kwenye duka hilo lililopo Mtaa wa Mpanda Hoteli Polisi walipata taarifa ya tukio hilo na walimkamata marehemu huyo na kumweka mahabusu hadi siku iliyofuata mchana.

Amefafanua kuwa kabla ya marehemu kufanya kitendo hicho cha kujinyonga alikuwa ametokea kituo cha Polisi Wilaya ya Mpanda alipokuwa amekwenda kuripoti kama ambavyo alikuwa ametakiwa na Jeshi hilo.

Mke wa Marehemu huyo Hawa Ayubu alisema kuwa yeye na marehemu walikuwa wakiishi kama mume na mke kwenye nyumba ambayo aliachiwa na mume wake ambae alifariki dunia na kumwachia nyumba hiyo ambapo kwenye maisha yake na Wile wamefanikiwa kuzaa mtoto mmoja wakike.

Amesema kuwa yeye alipigiwa simu na mume wake huyo ambae alimtaka awahi kurudi nyumbani kwamba alikuwa na shida nae ndipo alipofika nyumbani na kuingia ndani ya chumba walichokuwa wanalala alimwona mumewe akiwa ananing’inia juu ya paaa la nyumba kwa kutumia kamba huku pembeni kukiwa na situli pembeni ya kitanda.

Mmoja wa majirani Anastazia John anashuhudia kuwa walisikia mayowe ya Hawa Ayubu akipiga kelele ya kuomba msaada hali ambayo iliwalazimu wao majirani wafike kwenye eneo hilo na walipofika ndani ya chumba walikuta mwili wa marehemu ukiwa juu ya paa ya nyumba huku akiwa amejinyonga na mkewe akiwa amepoteza fahamu kutokana na mshituko wa kifo cha mume wake .



Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii