Katika tukio maalum lililofanyika ndani ya Kanda ya Ziwa, kampuni ya mawasiliano ya YAS imezindua rasmi kampeni yake kubwa iitwayo “Anzia Ulipo”, kampeni inayolenga kuwawezesha Watanzania, hasa vijana na wafanyabiashara, kutumia teknolojia kufikia ndoto zao popote walipo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa YAS Kanda ya Ziwa, Bwana Joseph Mutalemwa, alisisitiza kuwa kampeni hii si ya kawaida, bali ni mwendelezo wa safari ya mabadiliko ambayo YAS imeanza tangu ilipozinduliwa rasmi Novemba mwaka jana, ikibadilika kutoka chapa ya Tigo hadi YAS.
“Hayakuwa mabadiliko tu ya jina. Tulibadilisha kabisa namna tunavyowasiliana na wateja wetu. YAS iko kwa ajili ya kumsaidia mteja kufanikisha maisha yake ya kila siku awe ni kijana anayeanza biashara, mkulima kijijini, au mwanafunzi anayetafuta fursa kupitia mtandao,” alisema Mutalemwa.
“Sasa hivi hata ukienda kule kijijini kwa bibi yako, kama simu yako ina 4G, utapata 4G ya YAS. Na katika majiji kama Mwanza, Kahama, Shinyanga na Geita, tumeweka 5G katika maeneo haya,” aliongeza.