CCM Ruangwa yajivunia Majaliwa kuweka historia ya uongozi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi kimesema kinajivunia mwanachama wake, Kassim Majaliwa (64) kuweka historia ya kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa marais wawili.

Majaliwa alikuwa Waziri Mkuu wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, hayati John Magufuli na sasa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan.

Kiongozi huyo ametangaza kutogombea ubunge wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu. Wanachama watano wa CCM wilayani humo wamejaza fomu kuomba wateuliwe kugombea nafasi hiyo ili wapigiwe kura na wananchi kwenye kata 22 wilayani Ruangwa.

Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Abbas Mkweta amesema Rais Samia alikuwa na fursa ya kuchagua waziri mkuu mwingine lakini aliamua kuendelea na Majaliwa.

“Majaliwa ni mtoto wa Ruangwa, kwa hiyo sisi wana Ruangwa lazima tuseme asante kwa mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kumlea kijana wetu, kaka yetu, ndugu yetu Majaliwa Kassim Majaliwa kwenda naye mpaka hii term (awamu) sasa wanakwenda kumaliza wote,” alisema Mkweta.

Aliongeza, “ni heshima kubwa sana ambayo ametupa sisi wana Ruangwa kwa sababu uwaziri mkuu angeweza kuupeleka sehemu nyingine lakini ameamua kutupa sisi, kwa hiyo sisi kwetu unapozungumza habari ya mama Samia hiyo ni habari nyingine kabisa.”

Mkweta alisema Majaliwa ni kipenzi cha Watanzania, ni mkweli, anachukia rushwa, hapendi dhuluma, anapenda kuona maendeleo na anapenda kuona matokeo ya kinachofanyika.

“Usimuangalie Majaliwa kwa maana ya upana tu wa wana Ruangwa, ukitoa rais kwa wananchi, Majaliwa ni kiongozi anayeheshimika sana,” alisema alipozungumza na televisheni ya mtandaoni.

Mkweta alisema wananchi wa Ruangwa wameielewa falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya) ya Rais Samia na watampa shukurani katika masanduku ya kura wakati wa uchaguzi mkuu.

“Mama Samia hana sababu ya kuja kuomba kura, suala la kutafuta kura za Ruangwa atuachie sisi wenyewe, tutaifanya kazi hiyo na yeye atakuja kuyaona matokeo kwenye boksi,” alisema.

Julai 2 Majaliwa alitangaza analiacha jimbo hilo aliloliongoza tangu 2010 na akamshukuru Rais Samia na viongozi wakuu wa CCM kwa kumuamini na kumpa fursa ya kuwa Mbunge wa Ruangwa.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM taifa ameshukuru wananchi kwa kumuunga mkono wakati wote ambao amekuwa mbunge wa jimbo hilo.

Amewasihi wana-Ruangwa waendelee kuwa wamoja na siku ya uchaguzi wachague wagombea watakaowakilisha CCM.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii