RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ametajwa kuwa kinara namba moja wa uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia Afrika na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Nishati na Maji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Pongezi hizo zimetolewa Julai 3, 2025 na Viongozi mbalimbali na Wataalam kutoka Nchi nane za (SADC) ambao wamekutana jijini Harare nchini Zimbabwe katika Mkutano unaolenga kuimarisha na kujadili masuala mbalimbali yatakayowezesha mtangamano wa Kikanda katika sekta za nishati na maji.
Akizungumza Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa Serikali imeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia malengo yaliyoainishwa kwenye mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024 – 2034).
Kuhusu utekelezaji wa nishati safi ya kupikia kwa jumuiya hiyo, Kapinga ameitaka SADC kuweka dhamira na mikakati ya utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia ili kuwafikia watu wengi zaidi SADC.
Naye, Waziri wa Nishati wa Malawi, Ibrahim Matola amempongeza Rais Samia kwa uthubutu wake wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Watanzania. Matola ameitaka SADC kuitumia Tanzania kama balozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jumuiya hiyo.
Mkutano huo umehudhuliwa na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Suzan Kaganda, Wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme, Mha. Styden Rwebangila, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji (TPDC), Derick Moshi, Mkurugenzi wa Mifumo ya Udhibiti Umeme (TANESCO) , Mha. Deogratius Mariwa, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi (EWURA), Msafiri Mtepa na Wataalam kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.