Ueledi, ufanisi na maadili vyatakiwa kwa Watumishi wa Umma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, ametoa wito kwa watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi, na kuzingatia maadili, akisema kutofanya hivyo kumesababisha malalamiko ya wananchi kufikishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maswi ametoa wito huo alipokuwa akifunga rasmi mafunzo elekezi kwa wafanyakazi 79 kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Haki za Binadamu. Mafunzo hayo ya siku tatu yalifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.

Amesisitiza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kuwa waaminifu kwa serikali, kufanya kazi kwa weledi, kutumia vizuri muda wa kazi, na kuzingatia maadili ya kazi. Ametaja pia umuhimu wa kujiepusha na vitendo vya rushwa na ufisadi, kutunza siri na taarifa za serikali, kuwahi kazini, na kushirikiana kwa pamoja ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga uaminifu kwa serikali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu kutoka Tume ya Haki za Binadamu, Gabriel Rhobi, ametoa shukrani kwa Katibu Mkuu kwa kuruhusu na kufanikisha mafunzo hayo. Amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo washiriki wote na tayari ameona mabadiliko chanya, hasa katika upande wa maadili na mavazi.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii