Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church, maarufu kama Kanisa la Ufufuo na Uzima, limefungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, likiomba amri ya muda ya kuondoa zuio lililowekwa na Serikali dhidi ya kuendelea kwa shughuli zake za kidini, huku ikiripotiwa takribani maaskofu 500 wamefika kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo inalenga kulinda hadhi ya usajili wa kanisa hilo huku rufaa dhidi ya zuio hilo ikiendelea kusikilizwa.
Kanisa hilo linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia CCM.
Hivi karibuni mamlaka za Serikali zilifunga kanisa hilo kwa madai kwamba linaendesha shughuli kinyume na masharti ya leseni ya usajili wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mamlaka baadhi ya shughuli zinazofanyika ndani ya kanisa hilo zimeelezwa kuwa ni za kisasa kupita kiasi na hazilingani na malengo ya asili ya taasisi hiyo kama ilivyosajiliwa.
Kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala kanisa hilo limewasilisha shauri namba 13189 la mwaka 2025 dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msajili wa Taasisi za Kiraia.
Katika shauri hilo Glory of Christ Tanzania Church inaiomba mahakama kutoa amri ya muda itakayoruhusu kuendelea kwa ibada na shughuli nyingine za kidini, hadi pale rufaa iliyowasilishwa kupinga hatua ya serikali kufungia kanisa hilo itakaposikilizwa na kuamuliwa rasmi.