Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara imemfikisha mahakamani tabibu wa kituo cha Afya Magena kilichopo wilayani Tarime, Jacob Wankyo kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ili aweze kutoa huduma kwa mgonjwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mtuhumiwa huyo amefikiswa katika mahakama ya wilaya ya Tarime mkoani Mara jana Juni 10, 2025 ambapo mtuhumiwa alisomewa shtaka la kuomba rushwa ya Sh350,000 ili aweze kutoa huduma kwa mgonjwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Mwendesha Mashataka wa Takukuru Willim Lyamboko amesema mtuhumiwa huyo aliomba kiasi hicho cha fedha ili aweze kumfanyia upasuaji wa uzazi mgonjwa huyo aliyekuwa akihitaji upasuaji wa dharura kutokana na changamoto ya uzazi iliyokuwa ikimkabili.
Hata hivyo Lyamboko amedai Wankyo alipokea kiasi Sh200,000 ili aweze kutoa huduma hiyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 329 kifungu cha 15(1)(a) na (2).
Baada ya kusomewa shtaka lake kwenye kesi hiyo yenye namba 13960/2025 Wankyo amekana tuhuma ya kutendeka kwa kosa hilo.
Hakimu anayesikilza kesi hiyo, Veronica Selemani alisema dhamana katika shauri hilo iko wazi kwa masharti ya mshatkiwa kuwa na wadhamini wawili ambapo kila mmoja anatakiwa kusaini fungu la dhamana ya Sh4 milioni.
Aidha mtuhumiwa ametimiza masharti ya dhamana ambapo kesi hiyo imeahirishwa na itasikilizwa tena mahakamani hapo Juni 26 2025 kwaajili ya kusoma hoja za awali.