Iran yafanya mashambulizi Hospitali ya Israel na kusababisha majeruhi

Kombora lililorushwa kutoka Iran limelenga jengo la hospitali kuu ya Beersheba iliyopo kusini mwa Israel na kusababisha majeruhi kadhaa, huku yenyewe ikijibu kwa kushambulia mtambo wa urutubishaji nyuklia.

Mamlaka nchini humo zimethibitisha kuwa Iran imefanya shambulio hilo asubuhi ya leo Alhamisi Juni 19, 2025, huku taarifa zikisema bado tathmini ya madhara zaidi yaliyosababishwa na kombora hilo inaendelea.

Ofisa kutoka Idara ya Dharura ya Israel, Magen David Adom ameieleza Associated Press kuwa makombora mengine ya Iran yalipiga kwenye majengo mawili jijini Tel Aviv nchini humo na kujeruhi watu 40.

Kombora hilo lilitua Kituo cha Matibabu cha Soroka, ambacho huwadumia wagonjwa wengi Kusini mwa Israel.

Taarifa ya hospitali hiyo ilisema kuwa sehemu kadhaa za jengo hilo ziliharibiwa na kwamba kuna majeruhi wanaoendelea kupatiwa matibabu.

Hospitali hiyo ilifungwa kwa muda ili kuzuia wagonjwa kuingia isipokuwa kwa wale walioko kwenye hali mbaya. Haikufahamika mara moja idadi ya watu waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaani shambulio hilo na kuahidi kulipiza kisasi huku akisema Madikteta wa Iran wataadhibiwa kulingana na gharama za matendo yao.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii