Afisa wa polisi afyatua risasi kiholela, maandamano yaongezeka Nairobi

Nchini Kenya, mji mkuu wa Nairobi umetikiswa siku ya Jumanne, Juni 17, na makabiliano kati ya waandamanaji, vikosi vya usalama, na makundi ya raia wenye silaha, waliotajwa kuwa "majambazi." Watu kadhaa wamejeruhiwa. Waandamanaji hao walikuwa wamekusanyika kudai haki kwa Albert Ojwang, mwalimu aliyefariki mapema mwezi Juni alipokuwa kizuizini. Lakini hali wasiwasi ilizidi kutanda.

Mamia ya wanaume waliokuwa wamejihami kwa fimbo na mijeledi mapema asubuhi walifika kwa pikipiki katikati mwa jiji la Nairobi na kuwashambulia waandamanaji. Waandamanaji walijibu, wengine wakichoma moto pikipiki.

Wakati huo huo, vikosi vya usalama viliwakandamiza vikali waandamanaji. Kanda ya video ilisambaa ikimuonyesha afisa wa polisi aliyevalia zana za kutuliza ghasia akimpiga risasi raia mmoja kichwani.

"Polisi wanatakiwa kutulinda"

"Polisi wana matatizo gani? Tunaandamana kwa amani, na wanarusha mabomu ya machozi. Tuna amani, sina hata simu hapa, wala silaha sina," amesema Dennis, ambaye alikuwepo pamoja na Sayialel, wote wakiwa na mabango ya kumuenzi Albert Ojwang, aliyefariki akiwa kizuizini mwanzoni mwa mwezi Juni. "Kila wakati tunapoandamana, polisi huzua fujo kwa kurusha mabomu ya machozi au kuleta 'majambazi,' wakati polisi wanapaswa kutulinda wakati wa maandamano ya amani," Sayialel amesema.

Katika taarifa iliyotolewa jioni, polisi wamethibitisha kwamba mmoja wa maafisa wake "alimpiga risasi raia ambaye hakuwa na silaha kwa kutumia silaha ya kuzuia ghasia," na kuongeza kuwa afisa huyo amekamatwa. Taarifa hiyo pia imetaja uwepo wa "majambazi walio na silaha ghafi" ambao, kulingana na mamlaka, "watashughulikiwa kwa uthabiti." Wanaharakati kadhaa walishutumu majambazi waliotumwa na mamlaka.

Mmoja wa "majambazi," aliyeshikilia fimbo, alithibitisha bila kujitaja jina kwa shirika la habari la AFP kwamba aliahidiwa shilingi 1,000 za Kenya, au takriban euro 7, kwa uwepo wake "kulinda biashara."


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii