Mhubiri mwenye utata nchini Kenya afariki dunia

Mhubiri mwenye utata kutoka Kenya, Gilbert Deya, amefariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Jumanne jioni karibu na mji wa Kisumu, magharibi mwa Kenya.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, Deya alifariki papo hapo baada ya gari lake kugongana na basi la chuo kikuu pamoja na gari jingine. Ajali hiyo imesababisha majeruhi  takriban  30, wakiwemo mke wa Deya na wanafunzi 15 waliokuwa katika basi hilo.

Gilbert Deya alipata umaarufu mkubwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kudai kuwa ana uwezo wa kuwasaidia wanawake kupata mimba za kimiujiza kupitia maombi katika kanisa lake lililokuwa mjini London Uingereza.

Hata hivyo madai hayo yalizua maswali mengi na kupelekea kufunguliwa kwa uchunguzi uliomhusisha na mtandao wa ulanguzi wa watoto. Baada ya mvutano wa muda mrefu wa kisheria, alikamatwa na kurejeshwa Kenya takriban miaka minane iliyopita.

Mnamo miaka miwili iliyopita, Deya aliachiwa huru baada ya mahakama kuondoa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Kifo chake kimehitimisha safari ya maisha ya mtu aliyekuwa maarufu kwa matamko tata na anayebishaniwa sana kwenye medani ya dini Afrika Mashariki.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii