Tanzania yaanza kusaka suluhu kuhusu tahadhari ya Marekani

Serikali ya Tanzania imeanza kufanya mashauriano na Marekani ili kufanyia kazi maeneo yanayihitaji kuboreshwa ili raia wake wasizuiwe kuingia Marekani.
Uamuzi huo unatoana na Serikali ya Marekani kutoa orodha ya baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ambazo raia wake wanaweza kukutana na marufuku hiyo.

Taarifa ya zuio hilo la Serikali ya Marekani inayoongozwa na Rais Donald Trump ilitolewa hivi karibuni ikihusisha nchi 25 za Afrika, ilidai kutaka kuchukua hatua hiyo kwa kile ilichokieleza udanganyifu wa taarifa za raia wa nchi hizo.

Leo Juni 18, 2025 Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Gerson Msigwa ametoa taarifa kwa umma akisema imeona tangazo la Serikali ya Marekani la kutaka kufanyiwa kazi kwa mambo kadhaa ya kiuhamiaji ambayo yanaweza kusababisha raia wa Tanzania kuzuiwa kuingia Marekani.

Hivyo ameomba kuujulisha umma kuwa tayari Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imeanza kufanya mashauria na wenzetu upande wa Marekani kujua maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa maboresho hususani yanayohusiana na masuala ya kikonseli iii kuharakisha Tanzania isiwe moja ya nchi ambazo raia wake watazuiliwa kuingia Marekani.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ameongeza: “Tutaendelea kutoa taarifa kadiri majadiliano yanavyoendelea.
Baadhi ya mambo ambayo Trump hadi sasa amezuia ni pamoja na kuzuia ufadhili wa dawa za Ukimwi, kulazimisha kujisajili wahamiaji bila stakabadhi, kupunguza haki za umma kwa wahamiaji.

Pia amesitisha upatikanaji wa uraia kwa watoto waliozaliwa Marekani kwa wazazi wasio raia na ambao hawawezi kuthibitisha uraia wa baba.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii