Marekani yafahamu maficho ya Kiongozi Mkuu wa Iran

Mashambulizi ya kila upande kati ya Israel na Iran yameingai siku ya sita, huku Rais Donald Trump wa Marekani akitoa ujumbe  kuhusiana na mzozo huo mpya wa Mashariki ya Kati.

Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani inafahamu alikojificha Kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei katika kipindi hiki cha mzozo kati ya Israel na Iran, lakini hataki auawawe kwa sasa.

Katika ujumbe wake aliouchapisha kupitia mitandao ya kijamii, Trump ameitaka Iran "kusalimu amri bila masharti" huku mzozo huo ukizidi kuongezeka.

Mashambulizi baina ya nchi hizo mbili yameendelea yakiingia siku ya sita. Iran kwa mara nyingine imefyatua mkupuo wa makombora kuelekea Israel huku nchi hiyo nayo ikiushambulia mji mkuu Tehran na miji mingine ya Iran.

Hadi kufikia sasa watu waliouawa nchini Israel ni 24 na zaidi ya 600 kujeruhiwa. Na huko nchini Iran watu zaidi ya 200 wameuawa.

Wakati huo huo jeshi la ulinzi la Israel IDF limeripoti mapema asubuhi ya leo kwamba makombora zaidi kutoka Iran yanazidi kufyatuliwa.

Vingora vya tahadhari vilisikika huku jeshi la Israel likiwahimiza raia wake kufuata maelekezo yanayotolewa na idara ya tahadhari ya IDF.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii