Shirika la Afya Duniani (WHO) limeridhia rasmi Novemba 17 kila mwaka kuwa siku ya kuadhimisha watoto wanaozaliwa kabla ya kufikia muda kamili wa ujauzito, hatua ambayo imeelezwa kuwa na umuhimu mkubwa katika historia ya afya ya mama na mtoto.
Tangazo hilo limezua mwitikio chanya kutoka mataifa mbalimbali, huku Tanzania ikitajwa miongoni mwa nchi zilizochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mabadiliko hayo kupitia juhudi za muda mrefu katika huduma kwa watoto wachanga.
Katika ujumbe wake wa kuthibitisha hatua hiyo Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuwa kutengwa kwa siku hiyo maalum itasaidia kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu matatizo yanayowakumba watoto njiti pamoja na kuongeza msukumo katika uwekezaji na uboreshaji wa sera za afya kwa watoto hao.
Tanzania imejipatia heshima kubwa kufuatia kazi ya miongo kadhaa inayofanywa na Doris Mollel kupitia taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF). Doris, ambaye mwenyewe alizaliwa kabla ya muda, ameendelea kuwa sauti ya watoto njiti kupitia kampeni za kitaifa na utoaji wa vifaa tiba katika hospitali mbalimbali nchini.