Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu amesema siku ya Jumatano, Mei 28, kwamba Israeli imemuua Mohammed Sinwar, anayechukuliwa kuwa kiongozi wa Hamas katika eneo la Palestina lililoharibiwa na miezi 19 ya vita.
"Tumewatimuwa magaidi kutoka ardhi yetu, tukaingia kwa nguvu katika Ukanda wa Gaza, tukaangamiza makumi ya maelfu ya magaidi, tukamuua (...) Mohammed Sinwar," Benjamin Netanyahu ametangaza wakati wa kikao cha bunge.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israeli, shambulio la jeshi lililofanywa Mei 13 huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, lilimlenga Mohammed Sinwar, kaka yake Yahya Sinwar, kiongozi mkuu wa zamani wa Hamas, ambaye aliuawa huko Gaza mnamo mwezi Oktoba 2024 na kuonyeshwa kama mhusika mkuu wa shambulio la Hamas dhidi ya Israeli mnamo Oktoba 37, 20.
Kwa mujibu wa wataalamu wa vuguvugu la Kiislamu, Mohammed Sinwar alikuwa mkuu wa tawi la waasi la Hamas, Brigedi za al-Qassam.
Mashambulizi ya Israeli yameangamiza uongozi wa Hamas wakati wa vita vya miezi 19, na Mohammed Sinwar alikuwa mmoja wa viongozi wa mwisho kujulikana bado hai huko Gaza. Lakini kundi hilo la wapiganaji lilidumisha udhibiti wa maeneo ya Gaza ambayo hayakutekwa na Israeli. Hamas bado inashikilia makumi ya mateka na kufanya mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya vikosi vya Israeli.
Kama mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas, Mohammed Sinwar angekuwa na usemi wa mwisho juu ya makubaliano yoyote ya kuachiliwa kwa mateka, na kifo chake kinaweza kutatiza juhudi za Marekani na Waarabu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano. Israeli imeapa kuendeleza vita hadi mateka wote warejeshwe na Hamas washindwe, au kupokonywa silaha na kwenda uhamishoni.
Mohammed Sinwar alizaliwa mwaka 1975 katika kambi ya wakimbizi ya mjini Khan Younis. Familia yake ilikuwa miongoni mwa mamia ya maelfu ya Wapalestina waliofukuzwa kutoka eneo ambalo sasa linaitwa Israeli wakati wa vita vya 1948 vilivyofuatia kuundwa kwake.
Kama kaka yake mkubwa Yahya, Mohammed alijiunga na Hamas baada ya kuanzishwa kwake mwishoni mwa miaka ya 1980. Alipanda ngazi hadi kuwa mwanachama wa wale walioitwa Wakuu wa majeshi, nafasi sawa na kamanda wake wa muda mrefu, Mohammed Deif, ambaye aliuawa katika shambulio mwaka jana.