Wanamgambo wanane wanaoliunga mkono Jeshi la Nigeria kwenye vita dhidi ya makundi ya siasa kali wameuawa baada ya gari yao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika jimbo la kaskazini mashariki la Borno.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP wanamgambo waliuawa wakati wakirejea kwenye mji mkuu wa jimbo hilo Maiduguri wakitokea eneo la Ziwa Chad walikokuwa kwenye mapambano dhidi ya kundi moja la siasa kali lililovamia kambi ya kijeshi.
Katikati ya mwezi huu wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu Jimbo la Afrika Magharibi ISWAP waliivamia kambi ya kijeshi mjini Marte ambapo waliwauwa wanajeshi wanne kabla ya kuiteketeza kambi hiyo kwa moto.
ISWAP na kundi hasimu la Boko Haram wameendelea na mashambulizi yao kwenye majimbo ya Borno Adamawa na Yobe kwa miezi kadhaa sasa.
Mzozo huo wa miaka 16 umeenea hadi nchi jirani za Cameroon Chad na Niger na kupelekea kuundwa kwa muungano wa kijeshi wa mataifa hayo kukabiliana na wapiganaji wa siasa kali.