Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Jumanne Juni 10, 2025 inatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya kesi ya mgogoro wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, wanaojitambulisha kuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.
Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema ikiwa mdaiwa wa kwanza na Katibu Mkuu wa Chadema akiwa mdaiwa wa pili.
Sambamba na kesi hiyo, pia wadai wamefungua maombi ya zuio dhidi ya chama hicho kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi yao ya msingi itakapoamuliwa.
Hata hivyo Chadema imeweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo, huku ikitoa sababu tisa za kutaka kesi hiyo itupwe bila kusikilizwa madai ya msingi ya wadai.
Pingamizi hilo limejikita katika mamlaka ya Mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo haki ya wadai kufungua kesi hiyo matumizi ya sheria walizotumia kufungua kesi hiyo na uhalali kumuunganisha Katibu Mkuu.