Wakati viongozi wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) wakitua mkoani Kigoma kwa ajili ya mikutano mitatu kunadi operesheni ya Chauma For Change (C4C), Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla anaendelea kuchanja mbuga mkoani Kilimanjaro.
Viongozi wa Chaumma leo Jumatatu Juni 9, 2025 watafanya mikutano mitatu Kibondo, Uvinza na baadaye Kigoma Mjini ambapo itahutubiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe Kaimu Makamu Mwenyekiti Devotha Minja.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu hajaambatana na msafara huo, nafasi yake imezibwa na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Benson Kigaila.
Salum na baadhi ya viongozi wa chama hicho wamegawika kwenda Mkoa wa Katavi, wataungana na viongozi wenzao kesho mkoani Tabora.
Wakati huohuo Makalla anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro ambapo leo anatarajiwa kuhutubia wilayani Rombo.
Makalla alianza ziara ya siku saba katika mikoa ya kanda ya kaskazini kuanzia Juni 4,2025 ambapo alianzia mkoani Manyara alikofanya mkutano wa hadhara wilayani Babati kisha Arusha.
Ziara hiyo yenye lengo la kujibu kile alichokiita upotoshaji uliofanywa na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, John Heche ambao hivi karibuni walikuwa katika mikoa hiyo ya kaskazini.