Waumini 84 kati ya 86 waliokamatwa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, wameachiwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa kwa muda ambapo wakituhumiwa kukiuka maagizo ya Serikali.
Waumini hao ni miongoni mwa waliokamatwa alfajiri ya kuamkia Juni 3, 2025 kufuatia mvutano uliotokea kati yao na Jeshi la Polisi lililovamia makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam na kusitisha maombi yaliyokuwa yakiendelea baada ya Serikali kulitangaza rasmi kulifuta kanisa hilo.
Akizungumza na wakili wa Askofu Josephat Gwajima Peter Kibatala amesema jumla ya waumini 86 waliokamatwa miongoni mwao 84 wameachiwa kwa dhamana Juni 4 mwaka huu.
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro alipoulizwa kuhusiana na kuachiwa kwa waumini hao alijibu kwa kifupi kwamba kuna tofauti kati ya kukamatwa na kushikiliwa.