SHIRIKA la Umeme (TANESCO) limetakiwa kubuni vyanzo vipya vya umeme pamoja na kuendeleza kasi ya ukarabati wa miundombinu yake kwa haraka ili wananchi wote waweze kupata huduma bora ya Nishati.
Aidha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ametakiwa kupeleka umeme vijijini na kuviwezesha vijiji vyote kupata umeme pia kuendelea na kasi ya kupeleka umeme vitongojini.
Hata hivyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amezungumza hayo leo Juni 4, 2025 kufuatia na tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji wa Tathmini katika Wizara ya Nishati ambayo imeonesha kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2024/2025 utendaji kazi wa wizara/taasisi umeimarika kwa zaidi ya asilimia 95.
Hivyo Dk Biteko amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hususan REA, TPDC na TANESCO kuunganisha nguvu katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia ili ikue na kufanikiwa na hivyo kutimiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa wananchi wanahama kutoka kwenye matumizi ya mkaa.