TARATIBU ZA KUFUTA AU KUSITISHA UFANYAJI KAZI WA JUMUIYA AU TAASISI YA KIDINI

Nivema kutambua kwamba Katika muktadha wa Tanzania, utaratibu wa kisheria na kikanuni wa kufuta dhehebu au jumuiya ya kidini unategemea masharti yaliyowekwa chini ya sheria na kanuni husika na siyo hisia au msukumo wa kisiasa wa mtu na hasa kwa kuzingatia

1. Sheria ya Jumuiya za Kijamii (The Societies Act), Sura ya 337 (Revised Edition)

Sheria hii ndiyo inayosimamia usajili, uendeshaji, na uvunjaji wa jumuiya zisizo za kiserikali, zikiwemo jumuiya za kidini.

Mamlaka ya Msajili:

Msajili wa Jumuiya za Kijamii (katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) ndiye mwenye mamlaka ya kusajili na kufuta jumuiya, ikiwa ni pamoja na madhehebu ya kidini.Kwa hiyo kwa sheria hii anaweza kuonya,kuelekeza,au kusitisha lakini kwa kuzongatia masharti ya sheria na Katiba ya nchi.

Utaratibu wa Kufuata Kabla ya Kufuta Dhehebu:Msajili atatoa ilani au barua kuitaka dhehebu au taasisi

(i) Kuwasilisha Sababu za Kufuta (Section 12–14 of the Societies Act):
Msajili anatakiwa kuonesha sababu za kisheria zinazomfanya atake kufuta usajili wa dhehebu, kama vile:

1. Dhehebu limejihusisha na shughuli zisizo halali au za kuhatarisha usalama wa taifa;
2. Limeshindwa kufuata masharti ya usajili;
3. Linahatarisha amani, maadili au umoja wa kitaifa;
4. Limeshindwa kuwasilisha taarifa za kila mwaka kama inavyotakiwa.

Kuwasilisha Ilani
(Notice) ya Kufuta:

Kabla ya kufuta dhehebu, Msajili anatakiwa kutoa ilani rasmi ya maandishi (Notice of Intention to Cancel) kwa uongozi wa dhehebu husika, kwa kawaida kwa muda wa siku 30, akiwaeleza sababu na kuwapa nafasi ya kujibu au kujitetea.

Haki ya Kusikilizwa (Right to be Heard – Audi Alteram Partem):

Kwa mujibu wa kanuni ya haki ya kimsingi ya kisheria, dhehebu linapaswa kupewa haki ya kusikilizwa.

Msajili hana mamlaka ya kufuta bila kutoa fursa ya kusikilizwa kwa wahusika (fair hearing).

Mapitio au Rufaa ya Maamuzi (Judicial Review/Appeal):

Iwapo dhehebu linaona limefutwa isivyo halali, linaweza kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana na wasiporidhika kufungua shauri la mapitio (judicial review) katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga hatua hiyo,

Ufafanuzi wa Kikanuni (kwa baadhi yadhehebu):

Kwa madhehebu yanayohitaji kibali kutoka kwa taasisi nyingine (k.m. Baraza la Maaskofu CCT au  Mufti Mkuu), Msajili pia hufuata taratibu za kushauriana na vyombo hivyo kabla ya kuchukua hatua.

Taratibu zingine za ndani:
1. Ukaguzi wa mali na hesabu;
2. Mkutano wa wanachama kujadili hatma;
3. Kufungwa kwa ofisi rasmi.

MUHIMU:
Kwa mujibi wa sheria Msajili haruhusiwi kufuta dhehebu kiholela. Lazima afuate mchakato wa kisheria unaojumuisha ilani, sababu za msingi, haki ya kusikilizwa, na fursa ya kupinga maamuzi yake.

Kufuta bila mchakato huo ni kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 13(6)(a) kuhusu haki ya Kusikilizwa

Ili kupata taarifa zaidi endelea kutufuatilia kupitia website yetu ya www.jembenijembe.com kupitia Instagram ,Facebook, tikok,x zamani twitter pamoja na YouTube




Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii