Magari yanayotarajiwa kutumiwa na Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kwenye uzinduzi wa operesheni yake ya C4C katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo Jumatatu Juni 3, 2025 zikiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya kufungwa bendera za chama hicho.
Katika shughuli hiyo chama hicho kimeandaa magari matano aina ya Toyota Land Cruiser ambayo yamepambwa na rangi ya Chaumma pamoja na kufungwa bendera za chama hicho.
Miongoni mwa maandishi hayo yapo yanayosomeka, C4C (Chaumma For Change), yaliyo sambamba na maandishi mengine yalikolezwa kwa wino mweupe yakisomeka 'Tunaendelea Tulipoishia'.
Baada ya kumaliza kupambwa magari hayo yatakuwa yanazunguka viunga mbalimbali vya jiji la Mwanza kama mwanzo wa kuwapa taarifa wananchi kuhusiana na mkutano huo, ambao maandalizi yake yalianza wiki moja iliyopita.
Ingawa kabla ya kufanyika mkutano huo gari hizo zitaongoza maandamano ya wananchi na makada wa chama hicho yatakayoanzia maeneo ya Buhongwa, Mwanza.
Mbali na magari hayo msafara huo wa maandamano utasindikizwa na chopa iliyokodiwa kutoka Afrika Kusini kwenda viwanja vya Furahisha.
C4C baada ya kuzinduliwa leo inatarajiwa kuzunguka mikoa yote Tanzania kwa usafiri wa chopa, rasmi kwa utambulisho wa safu mpya ya uongozi wa chama hicho na kupokea wanachama wapya, kisha kuwaingiza kwenye mifumo ya katiba ya chama hicho.