Katika hali isiyo ya kawaida Kaburi linalodhaniwa kuwa amezikwa binadamu limekutwa katika shamba la viazi mtaa wa Edeni B kata ya Momoka manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa hali ambayo imezua taharuki miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo.
Majirani pamoja na Mjumbe wa serikali ya mtaa huo Bi Ashura Mbogela wameeleza namna walivyogundua uwepo wa kaburi hilo, kwamba walikuwa katika Upimaji wa njia mbadala itakayotumika kupita ndipo wakabaini uwepo wa kaburi katika shamba hilo.
Mmiliki wa shamba hilo Kheri Akili ambaye kwasasa anaishi katika mtaa wa bangwe kata ya Izia, amekanusha kuhusika na tukio hilo wala uwepo wa msiba katika familia yake kwa zaidi ya miaka miwili sasa na kuiomba mamlaka husika kufukua kaburi ili kubaini kilichomo ndani yake.
Taratibu za kufukua kaburi hilo zimefanyika mbele ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya sumbawanga Nyakia Ally Chirukile pamoja na diwani wa kata hiyo Charles chakupewa ambaye pia ni mchungaji, ambapo wamekuta sanda nyeupe bila uwepo wa mwili wa binadamu.