Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC inabainisha kwamba mahakama imeombwa kufutwa kwa vyama kadhaa vya siasa, ikiwa ni pamoja na kile cha PPRD cha Joseph Kabila. Uamuzi ambao upinzani unakiona kama vurugu za kisiasa, katika hali ambayo ni tete.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jahmuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jacquemain Shabani, amesema kuwa mahakama iepokea mashitaka ili kuomba kufutwa kwa vyama kadhaa vya siasa, ikiwa ni pamoja na kile cha PPRD (Chama cha Watu kwa ujenzi na Demokrasia), cha rais wa zamani Joseph Kabila.
Shughuli za chama cha PPRD zilisitishwa Aprili 19, baada ya kutangazwa kurudi nchini kwa Joseph Kabila kupitia Goma - mji ulio chini ya udhibiti wa kundi la waasi wa AFC/M23, linaloungwa mkono na Rwanda, kulingana na Kinshasa. Mnamo Aprili 24, ofisi ya mashtaka iliombwa kuanzisha utaratibu wa kuvunja chama hiki.
Mbali na PPRD, vyama vingine vitatu vinalengwa na ombi hili: ADCP, inayoongozwa na Corneille Nangaa, ambaye leo anagongoza kundi la waasi la AFC/M23, pamoja na CRP, chama kilichoanzishwa na Thomas Lubanga, ambaye hivi karibuni alitangaza kundi jimya la waasi huko Ituri, na MLP, chama cha mpinzani Frank Diongo, ambaye kwa sasa yuko uhamishoni nchini Belgique.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa DRC anasema vyama hivi vinaongozwa na viongozi ambao walivuka mstari mwekundu na wamejiunga na makundi yenye silaha yanayochukuliwa kama washambuliaji: "Ni juu ya vyama hivi kuchukua hatua watu hawa ambao wana kazi na majukumu katika vyama hivyo kujitenga na kulaani vitendo hivi vya kusirikiana na makundi ya waasi. La sivyo, sheria inatoa uwezekano wa kuvunjwa kwa vyama vyao.
Vyama hivi vinne vya siasa sio peke yao katika mtazamo wa mamlaka. Kulingana na Waziri, vyama vingine vimeonywa kwamba vinaweza kuvunjwa ikiwa "vitaendelea kutoheshimu makubaliano ya Jamhuri".
PPRD inalaani hila za kisiasa na kupinga utaratibu ambao umeanzishwa. Katibu wake Msaidizi wa Kudumu, Ferdinand Kambere, anapinga uhalali wowote katika mchakato huu:
"Sheria iko wazi: yule anayeomba kufutwa kwa vyama vya kisisa ni mwendesha mashtaka aliyefikishiwa malalamiko na uamuzi wa kuvunjwa kwa vyamahivyo. Sio waziri. Hatujawahi kuitwa kuhusiana na hilo, lakini kwa bahati mbaya, hadi leo, hakuna ofisi yoyote ya mashitaka iliyokiitisha chama cha PPRD."
Pia analaani uwepo wa polisi kwenye makao makuu ya chama hicho, jambo ambalo anaona ni kinyume na sheria: "Waziri wa Sheria ameweka polisi kwenye makao makuu ya chama chetu bila uamuzi wowote wa mahakama. Wanapaswa kutoka eneo hilo. Badala yake, kipaumbele kinapaswa kuwekwa katika uboreshaji wa hali ya kisiasa nchini. Anasema, bila shaka, ombi hili la kufutwa kwa chama cha PPRD ni "chokochoko dhidi Joseph Kabila".