Hospitali ya Upandikizaji Figo kujengwa Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki na  kushuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya ujenzi wa kituo kikubwa cha kupandikiza figo pamoja na utoaji mafunzo kwa madaktari bingwa ambacho kitakuwa ni kikubwa katika ukanda wa Jangwa la Sahara.

Kituo hicho kitajengwa kwenye Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ikiwa na lengo la ushirikiano kati ya Shirika la Tiba (TOKUSHUKAI) Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma na kinatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa msaada usiokuwa na masharti yoyote.

Utiaji saini huo umefanyika Mei 26, 2025 wakati kongamano la Biashara Uwekezaji na Utalii likiendelea lililowakutanisha  wafanyabiashara wa Tanzania, wafanyabiashara na wawekezaji wa Japan katika ukumbi wa mikutano katika Hoteli ya Westin Osaka, Japan, ambapo ni sehemu ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya World Expo Osaka 2025.

Akizungumza baada ya utiaji saini huo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa Profesa Abel Makubi amesema wamesaini makubaliano na shirika hilo linaloundwa na kundi la madaktari Wakijapan ambao wamekuwa wakisaidia utoaji na uboreshaji wa huduma za afya.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii