MADINI YENYE THAMANI YA BILLION 1.700 YAKAMATWA MWANZA

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Maafisa wa usalama kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za udhibiti wamefanikiwa kukamata madini ya almasi ghafi yaliyokuwa yanatoroshwa kinyume cha sheria na taratibu za usafirishwaji wa madini kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambapo madini hayo  yana thamani ya zaidi ya Tsh. bilioni 1.700.

Waziri Mavunde amesema hayo usiku wa kuamkia leo May 24,2025 wakati akiongea  na Waandishi wa Habari Jijjni Mwanza na kusema kuwa napenda kuutarifu umma wa Watanzania kwamba May 18, 2025 majira ya saa saba mchana, Maafisa wa usalama kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine za udhibiti walifanikiwa kukamata madini ya almasi ghafi yaliyokuwa yanatoroshwa kinyume cha sheria na taratibu za usafirishaji wa Madini kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Katika tukio hilo, almasi ghafi yenye uzito wa karati 2,729.82 na thamani ya takriban USD 635,887.66 (sawa na Tsh. 1,715,434,129.67) yaligunduliwa yakiwa yamefichwa kwenye mabegi manne na Raia mmoja mwenye asili ya India kwa lengo la kuyasafirisha bila vibali halali wala kufuata taratibu za kisheria.

Wizara ya Madini imesikitishwa na kuchukizwa na jaribio hilo la utoroshaji wa rasilimali za Taifa na inalaani vikali vitendo vya aina hiyo ikumbukwe kuwa utoroshaji wa madini ni kosa la jinai linaloikosesha nchi mapato na kudhoofisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla hivyo naomba nitumie nafasi hii kuufahamisha Umma kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika ili kubaini waliohusika na mtandao huu ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

Hivyo nawahakikisha kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kuhusika katika utoroshaji wa madini hayo ikiwa ni pamoja na kutaifisha madini hayo na kufuta leseni za kujishughulisha na shughuli za madini hapa nchini, Serikali haijalala na inaendelea kufanya oparesheni maalum usiku na mchana kubaini matukio yote ya aina hiyo nchi nzima ili kuendelea kulinda rasilimali madini yanayozalishwa nchini kwa manufaa ya Wananchi wa Tanzania na Taifa letu kwa ujumla.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii