Jeshi latakiwa kuwaachia huru wanahabari wanaozuiliwa

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) hapo jana Alhamisi lilitoa wito kwa watawala wa kijeshi wa Burkina Faso kuwaachilia huru waandishi watatu waliokamatwa wiki hii ambao wanazuiliwa katika eneo lisilojulikana.

Wito huo wa shirika la kutetea haki za binadamu unakuja wakati mamlaka ya Burkina Faso ikiendelea kusimamia ukandamizaji dhidi ya watu wanaoonekana kuwa wakosoaji wa serikali, baada ya kuchukuwa mamlaka mwaka 2022 kulingana na Human Right Watch.

Serikali siku ya Jumanne ilitangaza kuvunjwa kwa Chama cha Wanahabari wa Burkina (AJB), siku moja baada ya polisi kuwakamata rais wake, Guezouma Sanogo, na naibu wake, Boukari Ouoba.

Mwandishi wa habari wa tatu, Luc Pagbelguem, pia alichukuliwa kuhojiwa, kituo cha kibinafsi cha BF1 alichofanyia kazi ndicho kilitoa taarifa.

Kukamatwa huko kulifuatia hotuba ambayo Sanogo aliitoa kwenye kongamano la AJB wiki iliyopita ambapo alikosoa "mashambulizi dhidi ya uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari" nchini humo.

Human Right Watch imesema katika taarifa yake kwamba wenzake wa Sanogo na Ouoba walisema mawakili waliwatafuta katika vituo mbalimbali vya polisi na gendarmerie katika mji mkuu bila mafanikio na kwamba mamlaka imeshindwa kujibu rasmi maombi yao ya kupata taarifa na kwamba Mahali alipo Pagbelguem ambaye alikuwa ameripoti kuhusu matamshi ya Sanogo -- vile vile hapajulikani kulingana na ripoti hiyo.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii