Mwanamume Aliyehumukiwa Kifo Saudia Atarajia Kurejea Nyumbani

Stephen Munyakho, Mkenya aliyepatikana na hatia ya mauaji nchini Saudi Arabia, anatarajiwa kurejea Kenya kufuatia kuingilia kati kwa Jumuiya ya Waislamu Ulimwenguni. 

Machi 25, wakati wa futari katika Ikulu iliyoandaliwa na Rais William Ruto, katibu mkuu wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Hassan Omar, alithibitisha kuwa hatua hiyo ilifuatia mazungumzo yaliyofaulu. 

Omar alisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilimwalika katibu mkuu wa Muslim World League katika Ikulu, ambako Rais aliomba kwa dhati msaada kwa kesi ya Munyakho, ambaye alikuwa anakabiliwa na adhabu ya kifo kwa kosa la kumuua mwenzake. 

Alisema kuwa ombi lao liliheshimiwa pale shirikisho hilo lilipoingilia kati na kulipa fidia ya damu ya dola milioni 1—sawa na KSh 129.5 milioni—ili kuokoa maisha ya Munyakho. 

"Balozi wa Saudi Arabia nchini Kenya na balozi wetu nchini Saudi Arabia wamethibitisha kuwa ombi hilo limekubaliwa, na dola milioni 1 zimelipwa, hivyo Mkenya huyo atarejea nyumbani akiwa salama," Omar alisema. Katibu mkuu huyo wa chama tawala pia aliwataka Wakenya kuheshimu sheria za mataifa ya kigeni wanaposafiri nje ya nchi, akisisitiza kuwa ingawa serikali inaweza kuingilia kati, mamlaka yake yana mipaka. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii