Askari sita wa jeshi la Polisi la Kenya wameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulio linaloaminika kufanywa na kundi la kigaidi la Al-Shabaab la Somalia katika kambi ya polisi iliyoko kwenye kaunti ya Garissa mashariki mwa nchi hiyo, kwenye mpaka wa pamoja na Somalia.
Taarifa iliyotolewa na Polisi kwa vyombo vya Habari jana imesema, shambulio hilo lililotokea alfajiri ya kuamkia jana Jumapili lilifanywa na wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kundi la al-Shabaab la Somalia linaloshirikiana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Taarifa ya Polisi imebainisha kuwa, wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi walishambulia kambi ya askari wa akiba wakati wa alfajiri na walitumia silaha za aina mbalimbali kuvamia kambi hiyo.
Taarifa hiyo imeongezea kwa kusema: “Waliofariki sita wamethibitishwa na wanne wamejeruhiwa na wamelazwa hospitalini.”