Familia Ikifukua Mwili wa Marehemu Mchungaji Aliyezikwa Kisiri na Mkewe

Familia ya mwanamume aliyedaiwa kuzikwa kisiri na mkewe huko Voi, kaunti ya Taita Taveta, imechukua hatua kutokana na kucheleweshwa kwa haki.

Edward Mwaigo Maghanga alizikwa na mkewe bila idhini ya familia yake ya karibu.

Familia ya mchungaji huyo wa eneo hilo walikwenda mahali alipokuwa amezikwa ndugu yao na wakaufukua mwili wake ili kutuma ujumbe kwa wakwe zao. 

Mtumishi huyo wa Mungu kutoka kanisa la Deliverance for All Nations Church alizikwa wiki chache zilizopita baada ya mwili wake kudaiwa kuchukuliwa kutoka mochari.

"Nilienda kortini na kuomba nipewe mwili wa mwanangu, lakini niliambiwa hapana. Niliambiwa mwanangu atazikwa kwenye makaburi ya umma. Nilipinga na nikasisitiza kuwa mwanangu hatakuwa miongoni mwa waliozikwa pale," alisema Hana Malemba kwa uchungu.

Kwa sababu ya kucheleweshwa kwa haki, Malemba na familia yake waliamua kuchukua sheria mikononi mwao na kufukua mwili wa baba huyo wa watoto tisa.

Ilichukua saa tatu kuufukua mwili wa mchungaji huyo kutoka alikozikwa, ambaye alikuwa na mbavu 18 zilizovunjika.

Baadhi ya watu walijaribu kuzuia zoezi hilo la ufukuaji, ambalo lilifanyika bila kibali cha korti, bila usalama wala afisa yeyote wa serikali kuwepo.

Familia hiyo ililaumu mamlaka husika kwa kutokuchukua hatua kwa haraka na kufanya uchunguzi wa kina, jambo ambalo liliwapelekea kuchukua hatua hiyo kali. Malemba anapanga kufanya mazishi mapya kwa mwanaye huko Maktau na kumpa heshima anayostahili baada ya kisa hicho cha kusikitisha.

Familia hiyo inatarajiwa kufika mahakamani siku ya Ijumaa, Mei 16, wakiendelea kutafuta haki kwa jamaa yao ambaye anadaiwa kupigwa na kifaa butu kichwani. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii