Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limemfikisha mahakamani binti aliyejitambulisha kwa jina la Pendo Paul Elikana (19), mkazi wa Kijiji cha Mbuga ya Banya, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Katika taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Edith Swebe, imeelezwa kuwa binti huyo alitoa taarifa za uongo kuwa amepewa kazi ya kumuua kiongozi mmoja wa kisiasa.
Aidha, katika taarifa aliyoisambaza kwenye mitandao ya kijamii, alidai kuwa yeye ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo ambalo si la kweli.
Kamanda Swebe alieleza kuwa mara baada ya binti huyo kutoa taarifa hizo, uchunguzi ulianzishwa na kubaini kuwa taarifa zote alizotoa na kuzisambaza hazikuwa za kweli bali ni za uongo.
“Uchunguzi umebaini kuwa binti huyo hakuwa askari wa JWTZ kama alivyodai, bali alipata mafunzo ya mgambo. Hata hivyo, alitoa taarifa ambazo hazikuwa na ukweli wowote kuhusiana na tukio hilo,” alisema Kamanda Swebe.
Aliongeza kuwa uchunguzi huo umebaini kuwa binti huyo alifanya hivyo kwa maslahi yake binafsi na kwa nia ya kupotosha umma. Jeshi hilo limewataka wananchi kuacha kutoa taarifa za uongo, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Ikumbukwe kuwa katika maelezo yake, binti huyo alidai kuwa alipigiwa simu na mtu mmoja (jina linahifadhiwa) aliyemtaka aende kutekeleza shambulizi dhidi ya Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina.
Binti huyo alidai kuwa katika kutekeleza kazi hiyo, mtu huyo alimwahidi kumpa kiasi kikubwa cha pesa endapo angefanikiwa kutekeleza shambulizi hilo.
“Mtu huyo aliniahidi kuwa atanilipa pesa nyingi nikifanikiwa kutekeleza shambulizi hilo. Lakini nilikataa na nikamwambia kuwa siwezi kufanya hivyo, na hizo pesa zako wapelekee maskini,” alisema katika sehemu ya video hiyo.