Afisa wa kliniki katika hospitali ya Pandya amesimamishwa kazi kufuatia madai ya kusikitisha ya unyanyasaji wa kingono yanayohusisha mgonjwa wa figo.
Mshukiwa huyo aliyetambulika kwa jina la Dias Juma Wabwile alifikishwa kortini Jumatatu, Februari 3, akikabiliwa na mashtaka mawili ya ubakaji na kufanya kitendo kichafu na mtu mzima. Katika taarifa ya Jumatano, Februari 5, Baraza la Maafisa wa Kliniki (COC) lilithibitisha kupokea ripoti kutoka kwa vyombo vya habari kuhusu madai dhidi ya Wabwile.
Baraza lilithibitisha kuwa Wabwile ni afisa wa kliniki wa magonjwa ya nephrolojia aliyesajiliwa kwa nambari 20317. Licha ya kuwa hakuna malalamishi rasmi yaliyowasilishwa kwenye baraza hilo, timu imetumwa katika Hospitali ya Pandya kufanya uchunguzi wa kina.
Msajili na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza, Ibrahim Wako, alisisitiza kwamba maadili ya kitaaluma na uadilifu lazima izingatiwe katika nyanja ya matibabu. "Baraza la Maafisa wa Kliniki linalaani vikali aina yoyote ya vitendo visivyo vya kimaadili na uhalifu na limejipanga kuhakikisha wataalam wote wa afya wanazingatia viwango vya juu vya maadili.
Hadi sasa hakuna malalamiko rasmi ambayo yamepokelewa katika ofisi yetu. Hata hivyo, Baraza limetuma timu ya maofisa katika Hospitali ya Pandya kuanzisha uchunguzi wa kina ili Baraza lifanye uamuzi sahihi," alisema Wako.