Hali bado ni ya wasiwasi nchini Haiti kutokana na ghasia za magenge. Afisa wa polisi wa Kenya aliyetumwa Haiti, aliyejeruhiwa wakati wa operesheni, alifariki kwa majeraha siku ya Jumapili, Februari 23, Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MMAS), ambao kikosi cha Kenya ni sehemu yake, umesema leo Jumatatu Februari 24.
Licha ya kuwasili kwa maafisa wa polisi 1,000 kutoka nchi sita nchini Haiti, kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP, mashambulizi ya magenge, ambayo kulingana na Umoja wa Mataifa, yanadhibiti 85% ya mji mkuu wa Port-au-Prince, hayaonekani kuisha.
Afisa huyo wa kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni katika eneo la Arbonite, kaskazini-magharibi mwa kisiwa hicho, Kamanda wa MMAS Godfrey Otunge amesema katika taarifa. “Afisa huyo alisafirishwa kwa ndege mara moja hadi hospitalini (...) lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia,” ameongeza.
Mnamo Februari 16, maafisa wa polisi wa Haiti ndio ambao walikuwa waathiriwa wa shambulio la genge lenye silaha. Takriban maafisa watatu wa polisi waliuawa.
MMAS si kikosi cha Umoja wa Mataifa, lakini Umoja wa Mataifa umeanzisha mfuko wa hiari wa kufadhili, ambao hadi sasa umekusanya dola milioni 110, kiasi ambacho kinachukuliwa kuwa hakitoshi kabisa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alihakikisha mapema mwezi Februari kwamba Marekani itaendelea kuunga mkono ujumbe huo, siku chache baada ya Donald Trump kuamuru kusitishwa kwa jumla kwa misaada ya kigeni inayotolewa na nchi yake - mfadhili mkubwa zaidi duniani kwa dola. Mkuu wa diplomasia ya Marekani kisha akaidhinisha utoaji wa msaada wa kigeni wa dola milioni 40.7 kwa polisi wa kitaifa wa Haiti na Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MMAS).
Shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch kwa upande wake lilielezea wasiwasi wake kuhusu misheni na mashaka kuhusu ufadhili wake. Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishutumu polisi wa Kenya mara kwa mara kwa kutumia nguvu kupita kiasi na mauaji ya kiholela.
Takriban watu 5,601 waliuawa na ghasia za magenge nchini Haiti mwaka 2024, elfu moja zaidi ya mwaka 2023, kulingana na Umoja wa Mataifa. Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao, karibu mara tatu zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Siku ya Jumamosi, Januari 18, 2025 ilitangaza kutuma kikosi kipya cha maafisa wa polisi 217 nchini Haiti. Lakini kutumwa kwa mamia ya maafisa wa polisi wa Kenya nchini Haiti tangu mwezi Juni mwaka jana pia kumezua shutuma kali nchini humo. Chama kidogo cha upinzani, Third Way Alliance, kiliwasilisha pingamizi la kisheria mwezi Mei dhidi ya kutumwa kwa polisi wa Kenya, kikidai kuwa hakuna usalama nchini Haiti, hasa kaskazini.