Wanawake wawili wanauguza majeraha kutokana kisa cha kupigwa na mchungaji katika Kanisa la Betheli katika eneo la Kapkwen, Kaunti ya Bomet.
Waathiriwa, Mercy Rono (38) na Mercy Cherotich (30), walikimbia kutoka kwenye madhabahu ya kanisa hilo baada ya kushindwa kustahimili viboko.
Daktari Kelvin Kipchirchir kuwa shambulio hilo liliripotiwa kutekelezwa na pasta akisaidiwa na wahudumu wengine wa kanisa. Baadaye waliripoti kisa hicho kwa Kituo cha Polisi cha Kapkwen kabla ya kutafuta matibabu katika Kituo cha Afya cha Bomet. Afisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Bomet Felix Langat alithibitisha kuwa wanawake hao walipata majeraha mengi katika miili yao.
Washukiwa watoroka kanisani Kufuatia tukio hilo kamanda wa polisi kata ya Bomet Edward Imbwaga alitoa agizo la kufungwa kwa kanisa hilo mara moja huku polisi wakiendelea na msako wa kuwasaka mchungaji huyo na wenzake ambao walifanikiwa kutoroka.
"Tunachunguza hali ya usajili wa kanisa na jinsi limekuwa likifanya kazi kwa muda mrefu. Ripoti zinaonyesha kuwa waumini wake wengi ni wanawake," Kamanda Imbwaga alisema. Shambulio hilo limezua ghadhabu ya umma, huku wakaazi wenye hasira wakitishia kulibomoa kanisa hilo iwapo viongozi wataliruhusu kufunguliwa tena.