Mkuu wa Tume ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Volker Turk ameeleza kwamba watu 184 waliuawa wikendi iliopita nchini Haiti wakati magenge yenye silaha yalipoongeza kasi ya vurugu.
Utovu wa usalama nchini Haiti uliongezeka mwezi Februari wakati magenge yenye silaha yalipoanzisha mashambulio katika mji Mkuu wakitaka kuangusha utawala wa Waziri Mkuu Ariel Henry.
Makundi yenye silaha kwa sasa yanaripotiwa kudhibiti asilimia 80 ya maeneo ya mji Mkuu Port-au-Prince.
Licha ya kuwepo kwa kikosi cha polisi wa kimataifa kinachoongozwa na Kenya, machafuko yameripotiwa kuongezeka.
Mwezi Novemba, Umoja wa Mataifa katika taarifa yake ulieleza kwamba watu 4,544 waliuuawa katika mashambulio ya watu wenye silaha mwaka huu japokuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.
Machafuko nchini Haiti yanawalenga haswa wanawake na wasichana, waathiriwa wakikatwa kwa mapanga, kupigwa mawe na wengine kuchomwa moto au kuzikiwa wakiwa hai.
Zaidi ya watu laki saba wameripotiwa kutoroka machafuko, nusu yao wakiwa ni watoto kwa mujibu wa takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji IOM.