Mtoto wa mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma anayejulikana kwa jina la Jojo, Graison Kanyenye (6), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini usiku wa kuamkia Desemba 25, 2025 na kumwacha mtoto huyo chini ya usimamizi wa dereva bodaboda wa Ilazo Extension, Kelvin Gilbert.
Bodaboda huyo anayetajwa kuwa walimfahamu kupitia huduma ya usafiri wanayoitoa kwa familia, aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi wawili hao.
Mfanyabiashara maarufu kwenye mitandao ya kijamii aitwaye Chief Godlove amemlilia mtoto Grayson aliyeuawa kinyama jijini Dodoma na watu wasiojulikana.
Chief Godlove ameshea picha na video nyingi zikimuonesha akiwa na mtoto huyo akisema ni mwanaye wa hiyari ambapo ameandika;
“Nilikua bado siamini kama binadamu wamegeuka wanyama kiasi hiki hizi habari za binadamu waliogeuka wanyama kupoteza uhai wa mtoto asiye na hatia wala ugomvi na mtu yeyote hili jambo lisikie kwa watu wengine omba lisikukute tangu jana nimekaa napokea taarifa mbalimbali mitandaoni nikijaribu kukutafuta hata kumpigia simu mama yako simpati nikijarbu kutuma ujumbe hausomwi niko njiani kukuona mwanangu ulinipenda tulipendana ukaamua mimi niwe baba yako wa hiyari ni mwaka sasa sijakuona wengi husema hii ni mipango ya Mungu lakini binafsi hili limeniumiza limeniuma na sitaweza kulibeba kwa yeyote aliehusika hatakuja kuishi kwa amani kwenye hii dunia na akhera najua wewe ni malaika huna hata chembe ya ugomvi wala hasira umekuwa ukitabasamu na kucheka muda wote kama itakuwa ni mipango ya Mungu Mungu nisamehe lakini nafsi yangu inanambia Mungu hajaamuru binadamu kutoa uhai wa binadamu mwenzake kwa yeyote aliyehusika juu ya hili tunaiachia sheria ichukue mkondo wake na hata wakishindwa kupatikana miungu mungu na babu zetu hawawezi kuwaacha salama huko waliko Mungu ailaze mapema roho yako mwanangu baba yako nimeamua kuacha kila kitu nikufuate popote nikuage mara ya mwisho nakuahidi kama nitakuwa hai basi wale waliohusika ikishindikana mchana hata kwa maombi ya usiku watapatwa na chochote huko huko waliko r.i.p Greyson nakupenda nakufuata popote utakapokuwepo.”
Mbali na hilo, Jeshi la Polisi limesema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema Desemba 25, 2024 kuwa tukio litokea saa 1.00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.