Benki Kuu ya Tanzania imewataarifu Watanzania kuhusu zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985 hadi mwaka 2003 na noti ya shilingi mia tano iliyotolewa mwaka 2010.
Zoezi la ubadilishwaji linatarajia kuanza Januari 06, 2025 hadi Aprili 05, 2025 kupitia ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa.
Aidha Benki Kuu imesema matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia Aprili 06, 2025.
"Baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote duniani; na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko, " imeeleza taarifa ya Benki Kuu.