Jamaa mmoja jijini Dar es Salaam, Tanzania amejikuta pabaya baada ya mzigo wa mahindi aliokuwa ameiba kumkwama mabegani.
Frank Japhet, 23, mkazi wa Mbezi, jijini Dar es Salaam, amelazimika kujisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi, Kibaha, mkoani Pwani, baada ya mzigo huo kukataa kutoka mabegani.
Wakati akihojiwa kituoni hapo, mtuhumiwa amesema mzigo huo, uliokadiriwa kuwa na uzito wa kilo 20, uliofungwa kwenye gunia aliuiba kwa mama mmoja eneo la Mtaa wa Nyambwiro, Mlandizi, Kibaha, mkoani Pwani .
Mshukiwa huyo ameongezea kuwa, aliondoka na mzigo huo hadi eneo la kituo cha basi cha Mlandizi alinuia kuuacha kwa mwenzake ili arudie mzigo mwingine, na hapo ndipo mzigo huo ulikataa kutoka mabegani.
Kulingana na ripoti Japheth alikuwa bado ameubeba mzigo huo huku polisi wakisubiri mwenye mali auchukue. Polisi wamesema tayari wametuma taarifa kwa yeyote mwenye mzigo huo kufika kituoni hapo ili kuuchukua na kumnusuru Japheth.
“Ni kweli tukio hilo limetokea usiku wa kuamia leo, na hapa nipo kwenye kikao nikitoka tu nitafanya press (mkutano na wanahabari) kuhusu tukio hilo saa 7:30 mchana,” alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwanai, Kamishena Msaidizi wa Polisi (ACP) Jonathan Shanna Warioba