Mwenyekiti wa Chadema Kilimanjaro Akamatwa na Polisi Tuhuma za Kupanga Vurugu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Gervas Eliewaha Mgonja, (42), Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kutoa kauli za kuhamasisha Wananchi kuvamia makazi ya wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Simon Maigwa amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa baada ya kuonekana kwa video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii akiwa anawahamasisha wananchi kufanya uhalifu huo Novemba 27, 2024.

Maneno hayo ya kuhamasisha vurugu aliyatamka hadharani Novemba 24, 2024 na baada ya kutamka waliyasambaza katika mitandao ya kijamii.

SACP Maigwa ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo anachukuliwa maelezo ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii