Merz aonya kuhusu siasa za biashara

Kansela Friedrich Merz amesema Ulaya iko tayari kushirikiana na Asia kuimarisha biashara inayozingatia sheria huku akionya kuhusu athari za ushindani kati ya Marekani na China.

Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, ametumia siku ya mwisho ya ziara yake ya mataifa matatu barani Asia kutoa wito wa kuimarishwa kwa biashara huru duniani na kulindwa kwa mfumo wa uchumi unaozingatia sheria za kimataifa.

Akihutubia Mkutano wa Biashara wa Ujerumani na Ukanda wa Asia-Pasifiki mjini Seoul, Merz amesema ushindani unaozidi kuongezeka kati ya Marekani na China unaibadilisha kwa kasi mazingira ya biashara ya kimataifa kupitia ushuru, mikakati ya kutenganisha teknolojia na mbio za kutafuta malighafi muhimu.

Merz amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kushirikiana kwa karibu zaidi na mataifa ya Asia ili kuimarisha mfumo wa biashara unaotegemea kanuni badala ya nguvu za kisiasa. Amesisitiza kuwa nchi za Indo-Pasifiki, pamoja na Ujerumani na Ulaya, zinaathiriwa na mabadiliko hayo ya kimfumo katika uchumi wa dunia.

Kiongozi huyo wa Ujerumani amekosoa matumizi ya minyororo ya usambazaji na teknolojia kama nyenzo za mashinikizo ya kisiasa. Kwa mujibu wake, pale minyororo ya usambazaji inapogeuzwa "vita vya kibiashara na siasa" au upatikanaji wa teknolojia muhimu kuzuiwa, ustawi wa kiuchumi na usalama wa maeneo mbalimbali huwekwa hatarini.

Katika siku zilizopita, Merz ametembelea Singapore na Japan, ambako alisisitiza ushirikiano mkubwa wa kiuchumi kati ya Ulaya na Asia. Akiwa Singapore, alitoa wito wa kuanzishwa kwa makubaliano ya biashara huru kati ya Umoja wa Ulaya na CPTPP, muungano mkubwa wa biashara unaojumuisha nchi za Asia-Pasifiki na Amerika.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Korea KusiniHan Seong Sook amesema kampuni nyingi za Ujerumani zinaichukulia Korea Kusini kuwa kitovu muhimu cha kupanua shughuli zao katika eneo la Asia-Pasifiki.

Ziara ya Merz inakuja wakati mvutano wa kibiashara na ushindani wa kiteknolojia kati ya mataifa makubwa ukiendelea kuchochea mjadala kuhusu mustakabali wa biashara ya kimataifa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii