Akutwa amejinyonga mkoani Kilimanjaro

Mwanaume anayefahamika kwa jina la Hassan Ali anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 mkazi wa Pasua mkoani Kilimanjaro, amekutwa amefariki dunia kwa kile kinachohisiwa kuwa ni kujinyonga kwa kamba za katani pembezoni mwa uwanja wa Nelson Mandela, Pasua mjini Moshi.

Tukio hilo ni la tatu katika eneo hilo la Pasua kwa mwaka huu la watu kuchukua uamuzi wa kujinyonga kutokana na sababu mbalimbali.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa marehemu alikutwa asubuhi ya Novemba 14, 2024 akiwa amelala chini baada ya tawi la mti kukatika na kumbwaga chini huku wengine wakidai chanzo cha umauti ni kukata tamaa ya maisha na mahusiano ya kimapenzi.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro lilifika eneo la tukio baada ya wananchi kutoa taarifa kuhusu kukutwa kwa mwili huo katika eneo la Nelson Mandela ambapo hadi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina kutokana na utata kuwa alijinyonga au alinyongwa na watu wengine. 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii