Kijiji cha Ugenya, Kaunti ya Siaya, kimepigwa na mshangao kufuatia kifo cha watu wanne wa familia moja katika muda wa chini ya wiki mbili.
Wanafamilia watatu, akiwemo mama, mwanawe na mumewe, walifariki ndani ya siku tatu, huku mtoto wao wa mwisho akifariki wiki moja kabla yao.
Elly Otieno, jirani wa familia hiyo, alisema kuwa mama huyo aliyekuwa mjamzito alijifungua mtoto ambaye kwa bahati mbaya aliaga dunia siku moja baada ya kuzaliwa kwake.
Siku tano baadaye, mwanamke huyo pia aliaga dunia katika hali isiyoeleweka. "Mama alienda kujifungua, na mtoto alikuwa sawa baada ya kujifungua, lakini alifariki siku moja baadaye," Otieno alisema.
Familia ya Siaya yafariki katika mazingira ya kutatanisha Kulingana na Otieno, alikuwa akivuja damu nyingi baada ya kujifungua, lakini hawezi kuthibitisha ikiwa hilo ndilo lililosababisha kifo chake cha ghafla. “Mwanamke huyo alikuwa akitokwa na damu nyingi, lakini hakuna anayejua kama hicho ndicho kilisababisha kifo chake," alieleza.
Alibainisha zaidi kuwa mtoto wa kiume wa familia hiyo mwenye umri wa miaka 10 aliamka akiwa mgonjwa siku iliyofuata lakini hakufanikiwa kuona jua kwani pia alifariki. "Mwanawe, ambaye ana umri wa miaka 10, aliugua ghafla na akafa siku moja baada ya kutangazwa kuwa amekufa," jirani huyo aliongeza. Akiwa amehuzunishwa na kifo cha ghafula katika familia yake, mume wa mwanamke huyo aliugua, akionyesha dalili sawa na za mwanawe.
Alikimbizwa hospitalini lakini alifariki alipofika siku moja tu baada ya mtoto wake kufariki. "Siku moja baada ya kifo cha mwanawe, mkuu wa familia aliugua na kupelekwa hospitalini lakini alikufa alipofika," alisimulia.